Sunday, March 13, 2011

NENO LA JUMAPILI YA LEO

Kwa maoni yangu kama CCM itaendelea kuwepo madarakani daima dumu basi kuna maandishi ukutani yasomekayo, "TANZANIA HAITAENDELEA KAMWE", nasema hivyo baada ya kutaathimini kwa makini sana mwenendo wa mambo serikalini na kwenye chama hiki kikongwe Afrika.

Inawezekana kuna mazuri yanayofanywa na CCM, lakini sintajikita katika hilo

, maana naamini wapo watu walioajiliwa na chama kwa ajili ya kueneza uzuri wake kama vile akina TAMBWE, hii ni kazi ya akina Makamba ambao CCM kwa kiasi kikubwa inawaweka mjini.

CCM kamwe haijakwepa kasumba ya ukoloni ya kuwatukuza watu wachache na kuwasahau watu walio wengi.CCM ile ya mwaka 1967 si ya sasa, CCM ya Nyerere si hii ya Kikwete.CCM kimeendelea kuwa chama chama cha matajiri na kuwasahau wakulima na wafanyakazi ambao ndio msingi wa chama hiki kisichokuwa na mpango wowote wa kuwaletea maendeleo wananchi.

Sasa hivi kila mwenye ukwasi anakimbilia CCM maana anajua mali zake zitaendelea kuwa salama,matokeo yake serikali inashindwa kufanya maamuzi mazito,maana kuingia kwao madarakani ni matokeo ya ufisadi wa wakwasi hao ambao ndio wafadhili wakubwa wa chama.Chama kinabeba kila aina ya uchafu,kiasi kwamba ndani ya chama na serikali haonekani nani msafi na nani mchafu.

Wakulima ambao ndio msingi mkubwa wa CCM sasa hawathaminiwi tena,wao wamekuwa mtaji wa chama wakati wa uchaguzi baada ya hapo hawakumbukwi tena wanabaki wanatajwa tu kwenye hoja,lakini maisha yao ni yaleyale zaidi yanazidi kudidimia,hakuna matumaini yoyote kwa wakulima waliotapakaa kila pembe ya nchi hii.

CCM kimebaki kuwa chama cha kwenye makaratasi,na hata ukiwaangalia usoni wana CCM hawaonekani kama wanafanana.Wanatofautiana sana kimawazo na kimatendo,kila mtu na lwake.Hebu watazame kwa makini utangundua kuwa hakuna chochote kinachowaunganisha,wanashinda wanaparuana.Hata wale wanaonekana waadilifu kwa kiasi Fulani,hawaonekani,wamemezwa na uozo wa chama hiki,hakuna ambaye anaweza kunyoshea kidole mwanzake.

Ukitaka kugombea cheo chochote ndani ya CCM sharti uwe mkwasi,si mkulima na mfanyakazi kama awali,makundi haya hayana chao ndani ya chama hiki,wao ni daraja la kupandia kwa wenye nazo.Tangu Azimio la Arusha lizikwe huko Zanzibar,CCM ina wenyewe,wafanyabiashara ndio msingi mkubwa wa chama.Mchakato wa kugombea cheo chochote ndani ya chama hiki ni mzito mno kuliko ninavyoweza kusema.Aliyekuwa katibu mkuu wa CCM enzi za kibabe za Mkapa,bwana Philip Mangula amewahi kusema kuwa itafika muda kwenye uchaguzi ndani ya CCM itakuwa inatangazwa tenda ya kupata viongozi maana pesa ndio inayoamua nani wa kushinda.

Baadhi ya watu wanaosema ukweli ndani ya chama wanatengwa na hata kuadhibiwa kisirisiri mfano Samwel Sitta ambaye alianguliwa kwa mizengwe katika kinyang’anyiro za uspika.Hawataki utofauti wa mawazo,wanataka sauti za ndio mzee au zidumu fikra za mwenyekiti,kuna baadhi ya watu ni wamiliki wa chama na serikali.CCM wanaamini kuwa wao ndio wanaostahili kuongoza nchi,wana akili sana na ndio wanaojua sana matatizo yetu na masuluhisho yake.Wakijitokeza watu wengine wenye mwono tofauti wanapewa majina tofauti yanayochefua sana,wanasahau kuwa hii ni nchi yetu wote,hakuna anayeweza kusema yeye ni zaidi ya watu wengine.

Pengine hili ni suala la wakati,kama CCM wanaamini watabaki madarakani kwa sarakasi wanazofanya bila kushughulika na matatizo ya msingi ya wananchi wanajidanganya.Hawataki kusoma maandishi ukutani,ulevi wa madaraka umewatawala.Watanzania wengi wamechoka na maisha haya ya maigizo,pengine kinachosubiriwa ni mtu wa kuanzisha na kuongoza mapinduzi kama nchi za Kiarabu.Ole wenu CCM msipobadilika,kiama chenu kinakuja upesi,na hakuna atakayesalia,na kamwe hamtarudi tena,itabaki simulizi tu.

1 comment:

Anonymous said...

huo ndo ukweli wazee mimi najua ipo siku ccm haitaamini kitakachoitokea.. na bado kitambo kidogo tu hatutaiona tena, Amen.